MAONESHO YA TATU YA SIDO KITAIFA YAWA CHACHU YA UANZISHWAJI VIWANDA MKOANI KIGOMA

Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) katika kutekeleza Sera ya Viwanda Vidogo (SME Policy) na Mpango Mkakati wa Shirika limekuwa likihamasisha uanzishwaji na uendelezaji wa Viwanda Vidogo na vya Kati Nchini. Njia mojawapo ya kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda ni pamoja na kupitia maonesho yanayofanywa na SIDO pamoja na wadau  mbalimbali wa maendeleo nchini. Hii inatoa fursa kwa wananchi kuweza kupata nafasi ya kuona bidhaa na teknolojia mbalimbali zinazopatikana hapa nchi na hivyo kuchochea uanzishwaji wa viwanda vidogo na vya kati.
Maonesho ya kwanza ya SIDO Kitaifa  yalifanyika Mkoani Simiyu kwa kushirikiana na  Ofisi ya Mkuu mwaka 2018. Mwaka uliofwatia, 2019, maonesho ya Pili ya SIDO  Kitaifa yaliazimishwa Mkoani Singida kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida. Kutokana na ugonjwa ya UVIKO 19, maonesho ya SIDO kitaifa kwa mwaka 2020 hayakufanyika. Kwa Mwaka  huu 2021, maonesho ya  Tatu ya SIDO Kitaifa yamefanyika mkoani Kigoma kuanzia  tarehe 21 hadi 30 Septemba 2021 kwenye Uwanja wa Umoja mjini Kasulu – Kigoma ikiwa na waoneshaji wapatao 700 kutoka katika sekta mbalimbali za uzalishaji. 

Maonesho haya yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Philip Isdor Mpango, mnamo tarehe 22/09/2021 na kukaribishwa  na Waziri wa Viwanda na Biashara, Prof.Kitila Mkumbo;  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,  Mhe. Thobias Andengenye;  Mwenyekiti wa Bodi ya SIDO,  Prof. Elifas Bisanda;  na viongozi wengine mbalimbali. Kwa ujumla wao waliupongeza sana uongozi wa SIDO kwa kuandaa maonesho haya kwa kuwa yamekuwa ya tija kwa mkoa na kwa taifa kwa ujumla.

Katika hotuba yake, mgeni rasmi alifurahishwa na kaulimbiu ya maonesho haya ya SIDO ya “ Pamoja Tujenge Viwanda Kwa  Uchumi na Ajira Endelevu” kwa kuwa inalenga kutambua mchango wa Sekta ya Viwanda hususan viwanda vidogo na vya kati katika kuchochea uzalishaji kwenye sekta mbalimbali za Kiuchumi ili kukuza biashara ya ndani na nje, kuongeza ajira na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.

Mgeni rasmi aliongeza kuwa, maonesho ya viwanda vidogo na vya kati yana faida na umuhimu wa pekee kwa kuwa yanawezesha wenye viwanda kupanua wigo wa masoko ya bidhaa wanazozalisha  na hivyo kuongeza uzalishaji na kupelekea viwanda kukua. Maonesho yatatoa fursa kwa wenye viwanda kubadilishana ujuzi na uzoefu na hatimaye kuboresha bidhaa kulingana na mahitaji ya walaji na soko. Pia ni fursa kwa  wajasiriamali na wanachich kujionea wenyewe  mashine mbalimbali, vipuri na bidhaa ambazo zinatengenezwa hapa nchini, wapi zinapatikana na kwa bei gani.

Kwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Makamu wa Rais alielekeza Balozi zetu  zihakikishe kwamba utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi una lenga pia katika kukuza na kuendeleza viwanda vidogo na vya kati hapa nchini na  kusisitiza  kipaumbele kitolewe katika mambo yafuatayo:

(i) Kuvutia uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati, ili watu waje wawekeze hapa kwetu katika viwanda vidogo na vya kati;

(ii) Kuratibu upatikanaji wa teknolojia zinazofaa katika mazingira ya nchi yetu na masoko ya bidhaa za viwanda vidogo;

(iii) Kuratibu upatikanaji wa mitaji kutoka kweye mifuko au taasisi zinazofanya hivyo katika maeneo yenu ya uswawishi kule ambako Mabalozi wanatuwakilisha, hasa taasisi zinazotoa mikopo nafuu kwa taasisi ndogo ndogo hizi, lakini SIDO muungane nao katika hili, na nyinyi msisubiri tu Mabalozi tuowaagiza wafanye hivi, lakini nanyi muwasiliane na taasisi kama hizo, mnaweza kuwatumia Mabalozi lakini na nyinyi mhangaike;

(iv) Kuiunganisha Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo (SMEs) na zile za nje ili muweze kubadilishana uzoefu na taarifa za masoko pamoja na kuziwezesha kuingia makubaliano ya ushirikiano (MOU) katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na teknolijia na ubunifu; na

(v) Kuiunganisha Sekta ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo na taasisi zinazotoa elimu na kujenga uwezo kwa ajili ya SMEs zetu kuuza katika masoko ya kimataifa kwa kujua taratibu na kanuni zinazotumika katika masoko hayo.

Wadau mbalimbali waliweza kushiriki maonesho haya zikiwemo taasis za fedha kama NBC, NMB, CRDB, TCB, n.k. Pia taasisi za kiserikali kama TBS, TIC, NSSF, PASS, NEMC, EPZA, GSI, BRELA, TRA, na taasis zilizoko chini ya World Vision, UN n.k.  Huduma mbalimbali ziliweza kutolewa kipindi cha maonesho ikiwemo  utoaji wa leseni za biashara kupitia  BRELA na utoaji wa chanjo ya  UVIKO 19.  Baadhi ya bidhaa zilizokuwepo ni pamoja na bidhaa za uhandisi, vyakula vilivyosindikwa, bidhaa za mikono, bidhaa za ngozi, bidhaa za nguo, thamani mbalimbali n.k

Maswali mengi yaliyokuwa yanaulizwa na baadhi ya wakaazi wa Kigoma ni namna watakavyoweza kupata huduma mbalimbali zinazotolewa  na SIDO ili waweze kuzalisha bidhaa mbalimbali  kutokana na malighafi yanayotokana na mazao yanayopatikana kwa wingi  katika mkoa huo yakiwemo zao ya mchikichi, mihogo, asali na nta ya nyuki.