MASHINE ZILIZOTENGENEZWA NA SIDO ZAHAMASISHA WENGI KUANZISHA VIWANDA VIDOGO NCHINI

Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar Es Salaam (45th DITF)  yanayoratibiwa  na TANTRADE yalifanyika katika Viwanja vya Mwl. Julius Nyerere barabara ya Kilwa kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 13 Julai 2021. Maonesho hayo yamekuwa chachu kwa wananchi walio wengi waliopata fursa ya  kutembelea banda la SIDO katika kuanzisha viwanda vidogo. Watembeleaji hao walihamasika pale walipokutana na mashine mbalimbali zinazotengenezwa na  SIDO  kupitia  vituo vyake vya kuendeleza teknolojia (TDCs) kutoka katika baadhi ya mikoa ikiwemo Kilimanjaro, Arusha, Mbeya, Lindi na Iringa kama njia mojawapo ya  kuwatimizia ndoto zao za kuanzisha viwanda vidogo.

Mashine zilizokuwa katika maonesho hayo nyingi  zilikuwa ni za kuongeza dhamani mazao ya kilimo na baadhi ziliweza kukamilisha  mnyororo  mzima wa uzalishaji bidhaa.  Kwa mfano, kulikuwa na mashine za kubangua  karanga, kuchambua karanga, oven za kukausha karanga na mashine za kutengeneza siagi ya karanga.  Kwa kufuata  mnyororo huo huo,  kulikuwa na mashine ya kupukuchua mashindi,  kuondoa vumbi kwenye mahindi,  kukoboa na kusaga mahindi. Pia kulikuwa na mashine za mbao ambapo kwa mteja yeyote aliyetaka kuanzisha kiwanda cha kutengeneza thamani mbalimbali angeweza   kupata mashine ya kupasua mbao, kuranda, kuweka urembo n.k. Mashine nyingine zilizokuwepo ni pamoja na mashine za chaki, kusaga juisi za matunda mbalimbali, , kutengeneza matofali na  mashine za kukamua juisi za miwa.

Wajasiriamali katika fani ya uhandisi nao hawakubaki nyuma katika  ubunifu wa mashine mbalimbali  na hivyo   walikuja na mashine za  kutengeneza fencing wire, kuchakata mihogo, kutengeneza crisps za viazi, kutengeneza sabuni, kutotolesha vifaranga n.k.
Mashine hizi ziliwavutia wengi na kuona  kumbe dhana ya kuanzisha viwanda vidogo inawezekana ukizingatia malighafi zinapatikana kirahisi na teknolojia ya kuziongezea thamani ipo na niya ubora. Ili kuweza kuanzisha kiwanda kidogo kupata elimu ya kile utakachoenda kutengeneza ni cha muhimu sana. Hivyo washiriki wengi waliofika kwenye maonesho haya na kutembelea banda letu la SIDO waliweza kujiandikisha kwa ajili ya kupatiwa mafunzo mbalimbali yatakayowawezasha kuzalisha bidhaa zilizo bora. Wengine waliweza kupatiwa utaratibu wa kuanzisha viwanda ikiwemo mpangilio mzima wa  eneo la uzalishaji.

Oda mbalimbali ziliweza kutolewa  kwa watengenezaji wa mashine ambapo ilitupa picha kamili ya nini kitakachofuata  maonesho yajao  kwa kuwa tutakuwa na wajasiriamali wengi watakaokuja kuonesha bidhaa zao kwa kuwa wengi watakuwa wamepatiwa elimu na teknolojia bora zitakazowawezesha kuzalisha bidhaa zilizo bora na hivyo  kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Viwanda vidogo na vya kati na hivyo kupunguza umaskini kwa kiwango kikubwa.

PAMOJA TUJENGE VIWANDA