SIDO INAWEZA KUKUONGOZA NA KUKUFANYA KUWA MJASIRIAMALI MKUBWA NA MASHUHURI

Mama Celina chibanda ni msindikaji wa vyakula mkoani Iringa. Jina la biashara analo tumia ni MATEGEMEO VEGETABLES na bidhaa zake zinajulikana kwa jina la CHI PRODUCTS. Anasindika karanga, kitunguu saumu, soya ya chai na unga wa lishe. Alianza ujasiriamali mwaka 1998 kwa kufanya biashara ndogo ndogo za kutengeneza keki na kufunga karanga zilizokaangwa. Wakati wote huo alikuwa ameajiriwa.

Anasema mwaka 1999 alikutana na mjasiriamali anayeuza achali ya maembe, alianza kuwa mteja wake, lakini baada ya muda akamuuliza alikojifunza kutengeneza bidhaa yake. Mjasiriamali yule alimwambia kwamba , amepata mafunzo kupitia SIDO.

Mwaka 2000 alikuja SIDO Iringa kuuliza juu ya mafunzo na akapewa utaratibu, naye akaamua kujifunza usindikaji wa vyakula. Hivyo alianza kutengeneza siagi ya kuranga kupitia mafunzo. Anasema muda wote kila kukiwepo na mafunzo ya usindikaji hakukosa kujifunza.

Mwaka 2001 aliamua kuacha kazi na kufanya ujasiriamali kuwa ajira yake ya kudumu. Alianza kuzalisha akiwa yeye  na familia yake kwa kutumia mtaji wake wa mafao ya ajira.

Mwaka 2006 SIDO ilimuunganisha na mkopo kutoka EADB  ambao ulimsaidia kupata mashine ya kusaga karanga.  Pia mwaka 2009 alishiriki katika mradi wa  Busness Development Gateway (BDG) na alipata milioni nne laki nane, ambapo alinunua mashine nyingine  kubwa zaidi ya kusaga karanga pia.

Mwaka 2011 alianza kukopa SIDO kwa ajili ya kuwekeza katika vitendea kazi hasa mashine za kisasa zaidi, alikopa sh. 2,500,000 akanunua mashine ya kubangua karanga.

Mwaka 2015 alikopa sh. 3,500,000 akanunua mashine ya kusaga karanga na kusaga vitunguu saumu.

Mwaka 2017 alikopa sh. 3,500,000 kwa ajili ya upanuzi wa jengo la uzalishaji, ambalo lipo tayari na sasa kupitia mradi wa T-LED atapata ruzuku ya mashine ya  kisasa yenye uwezo  mkubwa wa kufanya mchakato wote wa karanga mpaka kufungasha.

Anasema SIDO mmemfanya kuwa mtu kwani kwa sasa, anasambaza bidhaa zake mpaka Mikoani kama vile Dar es Salaam, Dodoma na Mbeya. Akiwa ametoa ajira ya kudumu kwa watu watano (5).

SIDO imemsaidia kupata TBS na TFDA.

Anaishukuru sana SIDO kwa kumweka alipo kwa sasa, akiwa na jina hapa iringa la wasindikaji wakubwa wa vyakula.

 

 

Swahili
Main Image: