SIDO YAENDESHA MAFUNZO YA TOT ILI KUONGEZA WATAALAMU WENGI ZAIDI

Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), limeendesha mafunzo ya wiki tatu (tarehe 6 hadi 24 Aprili, 2021) kwa ajili ya wakufunzi  watakaokuwa wanatoa ushauri na mafunzo  kwa wajasiriamali nchini. Mafunzo yalifanyika na kuhudhuriwa na washiriki 52 waliotoka mikoa mbalimbali ya Tanzania bara katika ofisi za SIDO zilizopo Vingunguti – Dar Es Salaam.

Mafunzo yalifungwa na Eng. Prof. Sylvester Mpanduji (Mkurugenzi Mkuu wa SIDO) na alitoa pongezi kwa wahitimu kwa kupata utaalamu wa stadi tofauti tofauti za utengenezaji bidhaa.  Mafunzo hayo yaliendeshwa kwa nadharia na vitendo toka kwa wataalamu mbalimbali waliobobea katika utengenezaji vitu mbalimbali vikiwemo mivinyo, juisi, siagi ya karanga, sabuni za maji (za kunawa mikono, kufulia, kuoshea vyombo na za choo), sabuni za baridi na za moto za vipande( za dawa kufulia, kuogea n.k), utengenezaji wa mafuta  ya ngozi na nywele, uokaji  wa aina mbalimbali, utengenezaji wa maziwa ya mtindi, youghut, jibini, utengenezaji wa achari ya mbilimbi.

Wakufunzi walitoa changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo, ukosefu wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali kutokana na ushindani wa  bidhaa toka nje na hivyo kuiomba serikali kuweka mpango wa kuzuia bidhaa zinazotoka nje hasa zile zinazozalishwa na viwanda vyetu hapa nchini. Kuhamasisha watanzania kupenda vya kwao na hivyo kuinua uchumi wa nchi. Changamoto ya kutokuwa na eneo la uzalishia bidhaa hivyo kuwafanya wajasiriamali walio wengi kukosa  kupata vibali vya ubora wa bidhaa zao ikiwemo TBS.
Wakufunzi hao waliahidi kuwa mabalozi wazuri wa SIDO katika maeneo walikotoka na  kuahidi kutoa ujuzi na elimu waliyoipata ili kuwafikia watu wengi zaidi walioko mijini na vijijini.

Mkurugenzi Mkuuwa SIDO ambaye alikuwa mgeni Rasmi,  alifurahishwa na namna wakufunzi walivyojitokeza toka mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya kushiriki mafunzo haya muhimu. Aliwaasa wakufunzi kuhakikisha elimu hii waliyoipata ikawe chachu kubwa katika kuongeza thamani mazao yanayozalishwa hapa Tanzania kwa kuwa kumekuwepo na changamoto ya  upotevu wa mazao hasa ya kilimo na kupelekea nchi kwenye maskini. Alieleza kuwa asilimia 60ya bidhaa za vyakula vilivyosindikwa vinatoka nje ya nchi na hali hii itakomeshwa iwapo utaalamu uliotolewa kwa wakufunzi hawa utasambazwa kwa watanzania wengi na kuweza kutumia malighafi zinazozalishwa nchini kwa wingi na kuongeza bidhaa zilizosindikwa na watanzania sokoni.

Aliwaasa wajasiriamali kuendelea kufuata taratibu za uzalishaji  bidhaa mbalimbali zilizowekwa na TBS, BRELA, OSHA n.k  ili bidhaa hizo ziweze kukubalika katika masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.  Pia alieleza kuwa changamoto ya upatikanaji wa mikopo inakwamisha shughuli za wajasiriamali na kusema kuwa, sasa ufumbuzi umekwishapatikana baada ya mabenki mengi kutoa mikopo yenye riba nafuu zikiwemo benki za Azania na CRDB.