WAHITIMU WA VYUO KWENYE FANI YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA KUSAIDIA KATIKA UANZISHWAJI WA VIWANDA KUPITIA TAFITI MBALIMBALI ZINAZOFANYWA NA VYUO VIKUU

Katika kuhakikisha wahitimu wa vyuo katika nyanja za Sayansi na Teknolojia wanashiriki kikamilifu katika mchakato  mzima wa uanzishwaji  viwanda kupitia tafiti mbalimbali zinazofanywa na  vyuo vya elimu ya juu, SIDO kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST) wamesaini  Mkataba wa Ushirikiano (MoU) ili kuhakikisha ujuzi unaopatikana kutoka kwa  wahitimu haubaki kwenye mashelfu na badala yake unageuzwa  kuwa bidhaa / huduma inayouzika sokoni na hivyo kusaidia katika  mchakato  wa uanzishwaji viwanda nchini.  Ni dhahiri pia kuwa wahitimu wa vyuo vikuu wanaweza kuhamasishwa kwa urahisi katika kuanzisha, kukuza na kuendeleza viwanda ikiwa  yatakuwepo mazingira mazuri ya uwezweshaji  na upatikanaji wa  misaada  mbalimbali toka mashirika ya kiserikali na yale yasiyo ya kiserikali pamoja na taasisi za fedha.

Ushirikiano huu unakusudia kukuza matumizi ya maarifa yanayotolewa vyuoni ili kuchangia ajenda ya maendeleo ya taifa na kutoa fursa kwa taasisi za elimu kupata uzoefu wa huduma za viwandani kutoka kwa wajasiriamali wadogo na wa kati  ili kuboresha utoaji wa elimu kupitia tafiti kutokana na changamoto zinazoibuliwa. Hii itaongeza ushirikiano katika mafunzo, kutumika kwa matokeo ya tafiti na ushauri katika maeneo ya sayansi, teknolojia na ujasiriamali, ambayo ni nguvu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Katika ushirikiano huu MUST  ina uwezo wa kuleta  tafiti na ushauri wa maendeleo ya viwanda katika fani mbali mbali na SIDO ina uzoefu juu ya maswala ya maendeleo ya viwanda kupitia sekta ya ujasiriamali na uwezo wa utoaji huduma za  teknolojia, ukuzaji wa biashara, mafunzo, masoko na huduma za kifedha.  Pia SIDO ina nguvu ya mtandao mpana kupitia ofisi zake zilizopo mikoa yote ya Tanzania bara na wigo mkubwa wa  wajasiriamali na ushirikiano imara na wa karibu na taasisi za kuendeleza teknolojia ndani na nje ya nchi.

SIDO ni shirika linalotoa huduma mbalimbali kwa wajasiriamali  wadogo na wa kati nchini katika maendeleo ya teknolojia na viwanda; mafunzo, ushauri na huduma za ugani; masoko na uwekezaji na huduma za kifedha. SIDO inazo ofisi katika mikoa 25 ya Tanzania Bara na inamiliki vituo saba vya kutunza na kuzalisha teknolojia  (TDCs) katika mikoa ya  Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Kigoma, Mbeya, Lindi na Iringa. Pia inamiliki vituo vinne vya kutoa huduma za mafunzo na uzalishaji  (TPC) katika maeneo ya Dar Es Salaam, Singida, Dodoma, Mwanza, Kilimanjaro na Njombe.
MUST ni wataalamu  kwenye kufanya tafiti na kwenye ufundishaji na ushauri.  Pia wana nafasi nzuri ya kuzalisha wataalam waliohitimu katika nyanja mbalimbali  za Sayansi na Teknolojia.  MUST inao uwezo wa kufanya tafiti  na zipo tafiti mbalimbali zilizokwishafanywa  na  wahitimu wake  na wafanyikazi kupitia miradi iliyotengenezwa na wanafunzi ambayo inaweza kubadilishwa  kuwa bidhaa za ubunifu  / au huduma. Kwa kufanya kazi kwa karibu sana na MUST, SIDO inaweza kuchukua   tafiti hizo  na kuzifanyia kazi kwa kuzalisha  bidhaa  nyingi kulingana na mahitaji ya wateja.  

MUST inacho kituo cha kiatamizi na Uhamisho wa Teknolojia (CITT) chini ya  idara ya 'ubunifu na kiatamizi'  na 'Ujasiriamali na Usimamizi wa Biashara' ambapo SIDO nayo ina program ya kiatamizi ambapo   kazi kubwa ni kuhakikisha  mawazo ya kibunifu toka kwa wahitimu / vijana yanafanyiwa kazi na  kubadilishwa  kirahisi kwenda kwenye  bidhaa  inayouzika sokoni upitia huduma zinazotolewa kwa walengwa.
Mkataba huu wa ushirikiano  unalenga kushirikiana katika maeneo yafuatayo: -
(i)  Kusaidia kukuza mawazo ya ubunifu kupitia programu za kitamizi;
(ii)  Mafunzo, kutumia tafiti  zilizopo chini ya program mbalimbali na ushauri
(iii) Ubunifu katika bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali wadogo na wa kati,  teknolojia na michakato ya teknolojia.
(iv) Kushirikiana katika utaalam na uzoefu
(v) Kuomba fedha na kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali;
(vi) Kushirikiana kwenye matumizi ya vifaa kulingana  mahitaji;
(vii) Kuwapa ujuzi wanafunzi wanaotaka kujifunza kwa vitendo kupitia miradi na viwanda vinavyohudumiwa na SIDO. 
(ix) Sehemu nyingine yoyote inayohusiana na yaliyomo  hapo juu kama itakavyokubaliwa na pande zote mbili.

Makubaliano  ya ushirikiano yalisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Mhandisi. Prof.  Sylvester M. Mpanduji na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya, Prof. Aloyce Mvuma mnamo  tarehe 4 Februari, 2020 katika ofisi za SIDO Makao makuu - Dar Es Salaam.  Juhudi za pamoja za SIDO na MUST ni nguvu itakayosaidia na kutia chachu maendeleo ya   viwanda nchini. Utaratibu wa utekelezaji wa yaliyomo kwenye MoU hiyo unaandaliwa.