WAZIRI MKUU, MHE. KASSIMU MAJALIWA, AIPONGEZA SIDO KWA KAZI NZURI WANAYOIFANYA KWA WAJASIRIAMALI WADOGO NA WA KATI

WAZIRI MKUU, MHE. KASSIMU MAJALIWA, AIPONGEZA SIDO KWA KAZI NZURI INAYOIFANYA KWA WAJASIRIAMALI WADOGO NA WA KATI

Hii imejidhihirisha wazi, pale Waziri Mkuu alipofungua maonesho ya nne ya mifuko na program za uwezeshaji mnamo Februari 9, 2021 yaliyofanyika viwanja vya Sheikh Amri Abeid mkoani  Arusha. Katika ufunguzi huo, Waziri Mkuu alipata fursa ya kutembelea  mabanda mbalimbali na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na wajasiriamali wadogo na wakati. Alipata kujionea bidhaa mbalimbali zenye ubora wa hali ya juu ambapo alijaribu kuwahoji wajasiriamali kuhusu ujuzi na teknolojia wanazotumia ambapo walikiri kuzipata Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO). Alifurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na SIDO, na kutoa pongezi kwao kuendelea  kuwahudumia wajasiriamali zaidi na zaidi kwa kuwapatia huduma zitakazowawezesha kuzidi kusonga mbele na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

Pia Waziri Mkuu alisisitiza kwamba wajasiriamali waonyeshe kinagaubaga kuwa bidhaa hizo zimetengenezwa Tanzania, kwa kuandika ‘Made in Tanzania’.  Pamoja na kuweka picha ya bendera ya Tanzania, waongezee na maelezo hayo.
Maonesho hayo yalikuwa na takribani mifuko na program za uwezeshaji 25, taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi ambazo zinafanya shughuli za kuwezesha wananchi kiuchumi 77, pamoja na wajasiriamali 200 kutoka katika halmashauri mbalimbali na kutoka katika mikoa ya kanda ya kaskazini pamoja na kanda nyingine ambao nao walifika kuonyesha bidhaa zao.  

SIDO inatoa huduma zifuatazo mafunzo, teknolojia mbalimbali za mashine, utafutaji wa masoko ndani na nje ya nchi pamoja na utoaji mikopo.  Pia Shirika linaendesha program mbalimbali zikiwemo, Kitamizi (Incubator) yenye lengo la kuibua vipaji na mawazo ya kiubunifu kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza viwanda katika sekta mbalimbali, program ya mkakati wa wilaya moja, bidhaa moja na kongano.
Wajasiriamali wanakaribishwa kuja kujipatia huduma mbalimbali kupitia ofisi za SIDO zilizopo karibu yao. SIDO ina ofisi katika mikoa yote Tanzania Bara.  KWA PAMOJA TUJENGE VIWANDA!